WAHITIMU WA SHULE YA MSINGI YA MAZOEZI CHANG’OMBE WAREJEA SHULENI KUTOA SHUKRANI
WAHITIMU WA SHULE YA MSINGI YA MAZOEZI CHANG’OMBE WAREJEA SHULENI KUTOA SHUKRANI
Wanafunzi wa zamani waliohitimu katika Shule ya Msingi ya Mazoezi Chang’ombe kuanzia mwaka 2000, wametembelea shule hiyo tarehe 7 Agosti 2026 kwa lengo la kutoa shukrani kwa walimu wao pamoja na kuwatia moyo na hamasa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo kwa sasa.
Katika ziara hiyo, wahitimu hao walikabidhi mashine ya kuchapishia (printer) kwa ajili ya kusaidia shughuli za shule, sanjari na kutoa zawadi mbalimbali kwa mwalimu mmoja mmoja na wanafunzi, kama ishara ya kuthamini mchango mkubwa wa walimu katika kuwaandaa kwa maisha na mafanikio yao.
Aidha, wahitimu hao walipata fursa ya kushiriki chakula cha mchana pamoja na walimu wao, hatua iliyotoa nafasi ya kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya wanafunzi wa zamani, walimu na shule yao.
Ziara hiyo imeendelea kuonesha umuhimu wa wahitimu katika kuunga mkono maendeleo ya shule, huku ikiwahamasisha wanafunzi waliopo sasa kujitahidi katika masomo na kutambua thamani ya mchango wa walimu wao.