Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani katika Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE)
Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) kwa kushirikiana na Shule ya Msingi ya Mazoezi Chang'ombe kimeungana na ulimwengu mzima katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, katika tukio lililofanyika mnamo tarehe 5 Juni 2026. Maadhimisho ya mwaka huu yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Tuwajibike Kukijanisha Tanzania,” yenye lengo la kuhamasisha jamii na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na uboreshaji wa mazingira. Hafla hiyo ilipambwa na Mgeni Rasmi, Prof. Pendo S. Malangwa, Naibu Rasi (Mipango, Fedha na Utawala) wa DUCE, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo na shule, wawakilishi wa ofisi ya afya na mazingira, pamoja na wanachama wa klabu za mazingira kutoka shule za msingi, sekondari, na chuo.
Maadhimisho haya yalipambwa na shughuli mbalimbali za kimazingira na kijamii, yakianza rasmi kwa zoezi la upandaji miti lililoongozwa na Prof. Malangwa na viongozi wengine kama ishara ya kuunga mkono jitihada za uoto wa asili na kuifanya Tanzania kuwa ya kijani. Baada ya zoezi hilo, wanafunzi walitoa burudani zenye ujumbe mzito wa utunzaji wa mazingira kupitia mashairi na maigizo. Maigizo hayo yalijumuisha; igizo la madhara ya ukataji miti lililoongozwa na Amiri, igizo la umuhimu wa kutunza mazingira lililoongozwa na Kastory Kuguma, na athari za plastiki lililoongozwa na Janeth Mtweve. Aidha, kuonesha uwajibikaji kwa vitendo, mgeni rasmi alisisitiza washiriki wote kuwa mabalozi wazuri katika suala zima la usafi na kutunza mazingira.
Katika hafla hiyo, viongozi wa Klabu ya Mazingira DUCE, Jocktan Elias Mussa na Amani Dickson Yusuph, walisoma risala mbele ya mgeni rasmi iliyoeleza historia ya klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016 hadi kufikia wanachama 57 mwaka 2026. Pamoja na mafanikio makubwa ya kutoa elimu ya mazingira, risala hiyo ilibainisha changamoto kama uhaba wa fedha na mwingiliano wa ratiba za masomo kwa wanafunzi. Ili kukabiliana na hali hiyo, klabu ilipendekeza uwezeshaji wa kifedha, kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, kuanzisha warsha za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kutenga siku maalum ya usafi chuoni itakayoshirikisha jumuiya nzima.
Kwa ujumla, maadhimisho haya yameacha alama kubwa na kuonesha dhamira ya dhati ya DUCE katika kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa za kulinda ikolojia. Katika hotuba yake, Prof. Malangwa aliwakumbusha washiriki kuwa mazingira ndiyo uhai wetu, na dunia ni dhamana tuliyokabidhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo hivyo utunzaji wake haukwepeki. Kupitia ushirikiano wa wanafunzi, walimu, na wadau mbalimbali, tukio hili limefanikiwa kujenga uelewa mpana na kuacha wito mzito unaosisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa mazingira, ili kwa pamoja tuweze kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu isemayo, “Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”